Tunavyozidi kukaribia tarehe 7 Julai nakumbuka mwaka 2011, nilivoitwa na marehemu Waziri wa Michezo na Utamaduni, Bwana Joe Habineza na kupewa barua ya mwaliko ili niende Nairobi kwenye mkutano wa Kiswahili uliyoanzisha Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Africa chini ya ACALAN ikiongozwa wakati huo na Profesa Sozinho Matsinhe.
Kwa jazba na raha ya kumwona tena huyu ndugu Matsinhe akiwa Katibu Mtendaji, nikakumbuka enzi zetu tukiwa pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani na hotuba nzuri za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa Tanzania na mkuu wa Chuo (Chancellor).
Nakumbuka nikibabaisha Kiswahili na ndugu huyu akitokea Msumbiji (Mozambique) na mimi nikitokea Rwanda. Kama wasemavyo wasomi kweli Kitabu ni zawadi kubwa na ya kudumu katika maisha ya binadamu.
Nkrumah Hall, ambapo tulikua tunakutana kwa ajili ya chakula ndipo siku ya kwanza kabisa nikatoka nakuelekea duka la vitabu baada ya kusoma maoni ya marehemu Mzee PUNCH kwenye ukuta wa Cafeteria yetu hiyo.
Kitabu cha kwanza nilichonunua siku hiyo kilikua na maneno ya Mwalimu “Sababu tunayo, Nia tunayo, na Uwezo tunao”. Niliachana na marafiki zangu wengi kama Sewangi na wenzake mwaka 1986 na kuendelea na safari ya maisha huko Kenya nilipokutana na Ustadi Wallah bin Wallah, mwalimu aliyebobea katika Kiswahili.
Kukutana tena na huyu ndugu Sozinho 2011 baada ya robo karne na kumchagua ndugu John Kiango ambaye na yeye alikua mwanachuo hicho kutoka Tanzania kua Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, wote sasa wakiwa Maprofesa, tukiwa na ma Profesa Kimani Njogu na wengine kutoka Kenya, yote hayo yamenipa hamasa na slaha kubwa na bidii ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili nchini Rwanda.
Kwa heshima na taadhima, pamoja na jitihada zote nakumbuka maneno aliyoyasema mwenzetu Profesa Mutembei, tukiwa kwenye mkutano wa ACALAN, tukiwa Hotel Chez Lando, Kigali nchini Rwanda 2021 kwamba, Kiswahili kina maadui wengi kutoka ndani na nje kukipigania na kukipigia debe si kazi rahisi.
Na kweli kikulacho kinguoni mwako waswahili wamesema. Hii ni nafasi nzuri sana kutafakari maneno ya Profesa Iribe Mwangi kuhusu maandalizi ya SIKU ya KISWAHILI DUNIANI, kwa mara ya tatu yatakaoandaliwa na KAKAMA, ya kwanza yakifanyika Zanzibar, kufuatiwa na Kampala mwaka jana , na Kenya mwaka huu 2024.
Ni matumaini yangu kwamba siku hiyo ikiwa ni ya tatu ya Kongamano la kimataifa la Kiswahili litakaloanza tarehe 5 Julai huko Kenya kama taarifa niliyoipata niyauhakika itafana sana na kuamsha waswahili vijana waamke washike slaha za hekima, ujuzi, na teknolojia wazidishe ukuzaji na uendelezaji wa Kiswahili kama Utamaduni na Utambulisho wa Mwafrika.
Kwa Serikali ya Rwanda na Africa Mashariki nazidi kushukuru nikikumbuka mwaka 2014, nilipo wakilisha Rwanda kama mjumbe kuanzisha EAKC au KAKAMA. Tukiwa visiwani Zanzibar, tulikubaliana kuboresha ushirikiano na ushikamano kwa dhati kabisa.
Na kama wakati huo nchi za Jumuiya zilikua tano tu na leo hii ni nane, Mungu atupe nini zaidi ? Wadau na wapenzi wote wa Kiswahili haswa vijana, tafadhalini changamkeni, matunda yako mbele. Penye nia hapakosi njia, pamoja twaweza.
Profesa Pacifique Malonga,
Mwandishi na Mwanahabari, Kigali- Rwanda